Nchini Tanzania, uhuru wa kujieleza unalindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Katiba ya Zanzibar ya 1984.
Ibara ya 18 ya katiba ya Jamhuri na kifungu cha 18 cha Katiba ya Zanzibar, zinatoa uhuru kwa wananchi kutoa maoni yao na kuheshimiwa bila kuingiliwa.
Sambamba na katiba, ipo mikataba ya kimataifa na kikanda ambayo inalinda uhuru wa kujieleza.
Tamko la Ulimwengu la Haki za Binadamu (Universal Declaration of Human Rights 1948) pamoja na mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na haki za watu, kifungu cha 19 kinatoa haki na uhuru wa kila mtu kuwa na maoni yake na kujieleza na bila kuingiliwa.
Mikataba mengine inayolinda uhuru wa kujieleza ni Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (The African Charter on Human and People’s Rights (1981) na Tamko la kanuni za uhuru wa kujieleza Afrika (Declaration of Principles on Freedom of Expression in Africa).
Lakini jee haki ya uhuru wa kujieleza ina mipaka? Je sheria zetu zinaruhusu kukosoa serikali?,Jee uhuru wa kujieleza upo na unaheshimiwa? Ni wakati gani tunaweza kusema mtu amevuka mipaka ya uhuru wa kujieleza na kutenda kosa la uchochezi?.
Haya ni maswali muhimu kujiuliza kwa sababu sasa hivi tunapitia kipindi kigumu ambapo ni rahisi mtu kushtakiwa kwa kosa la uchochezi kwa kauli tu za kawaida kuhusu masuala ya umma.
Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 inasema: Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa njemawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.
Kwa bahati mbaya ibara hii haijawahi kutafsiriwa na mahakama ili kubainisha wigo wa uhuru wa kujieleza na wigo wa mipaka au masharti dhidi ya haki hii.
Matokeo yake ni kawaida kwa watu kukamatwa, kushtakiwa na kufungwa kwa kukosoa utendaji wa serikali.