SERIKALI imezindua zana kadhaa za kisheria huku nchi ikielekea kuwa sikivu zaidi kwa watu wenye ulemavu.
Zana za kisheria ikiwa ni pamoja na sera ya watu wenye ulemavu na sheria ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2022, zinaakisi azma ya serikali ya kuhakikisha watu wenye ulemavu wanaishi maisha sawa na makundi mengine.
Sheria mpya ya watu wenye ulemavu ya 2022 inatoa fursa na haki nyingi zaidi kwa watu wenye ulemavu ikilinganishwa na sheria Na. 9 ya mwaka 2006, ambayo licha ya kulalamikiwa lakini ilinyima haki na fursa nyingi kwa watu wenye ulemavu.
Kwa sheria hii mpya, sasa mzanzibari mwenye ulemavu anaweza kudai tafsiri ya lugha ya ishara kwenye mahojiano ya kazi.
Haki hii pamoja na nyengine, zimetajwa katika sehemu ya nne inayohusu haki na fursa, kuanzia vifungu vya 28 hadi 31 vya sheria.
Hata hivyo, haki kuwemo katika sheria ni sehemu moja na usimamizi na utekelezaji wa haki hizo ni jambo jengine.
Hivyo, bila usimamizi na utekelezaji wa sheria hii, haki na fursa zilizoanishwa kwa watu wenye ulemavu hazitakuwa na maana yoyote.
Hivyo, ni wajibu wa serikali, vyama vya watu wenye ulemavu na baraza la watu wenye ulamavu kuhakikisha sheria hii inatekelezwa na inakuwa jumuishi kwa makundi yote ya watu wenye ulemavu.
Sote tunawafahamu watu wengi wenye ulemavu wanaweza kufanya kazi na kutaka kufanya kazi na wana mengi ya kuchangia lakini hawajaajiriwa.
Miundombinu yetu ya ajira, nafasi za ofisi na teknolojia za mawasiliano mara nyingi hazijawekwa ili kushughulikia masuala ya ulemavu.
Ingawa sheria imekuja na mwarubaini wa changamoto hizi, bado utelekezaji na matokeo yanayotarajiwa yatategemea nguvu na ushawishi wa vyama vya watu wenye ulemavu na jinsi vitakavyosimama kutetea utekelezaji wa sheria hii kwa ukamilifu wake.
Kwa mfano kifungu cha 28(1)a watu wenye ulemavu wana haki ya kupata elimu ikijumuisha mafunzo ya amali na mafunzo ya kukabiliana maisha kulingana na aina za ulemavu.
Aidha, kifungu cha 29(1) kinatoa jukumu kwa Baraza la Watu Wenye Ulemavu kushajiisha ufikiaji wa miundombinu ya kijamii, kiuchumi, kiutamaduni, afya elimu, habari na mawasiliano ili kuwawezesha watu wenye ulemavu kufaidika kikamilifu na haki zote za binaadamu kwa kujitegemea.
Vifungu hivi ni muhimu sana kuwemo ikilinganishwa na mazingira ya sasa ya watu wenye ulemavu ambapo wanashindwa kuzifikia huduma mbalimbali ikiwemo elimu kutokana na mazingira ya ulemavu wao.
Aidha, wanakabiliwa na changamoto ya kuzifikia huduma za afya ambazo ni moja ya haki za watu wenye ulemavu zilizoanishwa katika sheria.
Hivyo basi, ni wajibu wa serikali na baraza la watu wenye ulemavu kuhakikisha miundombinu inayojengwa inakuwa rafiki kwa watu wenye ulemavu ili wazifikie huduma kwa wepesi.
Kwa muda mrefu, watu wenye ulemavu wameshindwa kutoa huduma bora na zenye tija kwa jamii na serikali kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ufinyu wa mafunzo, wakalimani wa lugha ya alama na kubwa zaidi miundombinu isiyo rafiki kwa kundi hilo.
Sheria pia imeweka wazi haki za watu wenye ulemavu kufaidika na fursa za kiuchumi. Hili ni eneo moja ambalo linalalamikiwa kwa muda mrefu na kundi hili, wakieleza jinsi wanavyotengwa na fursa za fedha zikiwemo zile zinazopaswa kutolewa na manispaa, halmashauri na mabaraza ya miji.
Hili ni eneo jengine ambalo serikali kwa kushirikiana na na baraza la watu wenye ulemavu kuliangaliwa kwa upana ili kupunguza malalamiko.
Ukiachia serikali na baraza, jamii pia ina wajibu wa kuwasaidia watoto wenye ulemavu ili waweze kuwa raia wenye manufaa.
Kama Zanzibar inataka kupata maendeleo jumuishi, watu wenye ulemavu wanastahili “fursa si kuhurumiwa”.